Kuongoza Kizazi cha Wanateknolojia kwa ajili ya Mazingira

Ni watu wachache sana wanaotambua mchango wa wanawake katika uhifadhi wa mazingira. Utafiti unaonyesha kuwa wanawake huathirika pakubwa na mabadiliko ya hali ya anga na majanga ya kimaumbile. Hata hivyo, vyombo vya habari mara nyingi huelekea kuwasawiri wanawake kama waathiriwa wa majanga yanayohusishwa na mazingira, bila kuangazia juhudi mbalimbali za wanawake, na hasa wasichana, katika kupambana na mabadiliko ya hali ya anga.

Mnamo mwaka wa 2016, nilihudhuria Kongamano la Wanawake na Wasichana Wapenda Teknolojia lililofanyika mjini Accra, Ghana. Nilishangazwa na idadi kubwa ya wanawake na wasichana wanaoongoza miradi mbalimbali ya kiteknolojia. Nilivutiwa sana na wengi waliotoa hotuba za kusisimua kuhusu jinsi ya kuifanya teknolojia kitu cha kuchangamkiwa na wanawake na wasichana. Niliingiwa na hamu kubwa ya kuchangia katika maendeleo ya kijamii kupitia teknolojia. Ilhamu yangu ikawa imepata mwamko wa ajabu.

Wakati huo ndipo Wakfu wa Let’s Do It ulipokuwa unamtafuta mtu ambaye angeongoza shughuli zake nchini Kenya. Nafasi yenyewe ilihitaji mtu mwenye ujuzi na uelewa wa mazingira na matumizi ya teknolojia ambaye angesaidia katika ukusanyaji wa data na kubainisha zilikokuwa sehemu za takataka kama njia ya kurahisisha uondoaji wa takataka hizo nchini kote. Sikuweza kukubali nafasi kama hiyo inipite.

Ni zaidi ya mwaka sasa na ninaweza kusema kwa hakika kuwa hiki ndicho kitu cha kuridhisha zaidi nilichowahi kufanya. Jukumu langu la kwanza kama kiongozi wa Wakfu wa Let’s Do It Kenya lilikuwa kufanyia majaribio kitumizi cha kiteknolojia cha shughuli za wakfu huo. Niliona fahari kuu kuwa miongoni mwa kundi lililofanya kila juhudi ili kuleta mabadiliko makubwa ulimwenguni. Kuweza kuchangia maoni na kutoa ripoti kuhusu mafanikio ya kitumizi hicho, jambo lililofanikisha kubuniwa kwa Kitumizi cha Kimataifa cha Usafishaji Mazingira, kulinipa furaha isiyomithilika.

Kuwa kiongozi wa kike wa umri mdogo hakujakuwa jambo rahisi. Unalazimika kuhakikisha kuwa kazi yako haina dosari. Jamii ina matarajio makubwa zaidi juu ya wanawake wanaoshikilia nafasi za uongozi kuliko katika wanaume. Pana mwelekeo wa kukashifu wanawake wanapofeli katika uongozi, jambo linalosababisha imani ya jumla kwamba wanawake hawawezi kuwa viongozi wazuri. Hivyo, nimejitahidi kufanya bidii ili kazi yangu iwe bora na kuniletea sifa nzuri.
Tangu nianze kutekeleza majukumu yangu katika Wakfu wa Na Tulitende, nimejiamini zaidi na sasa ninaweza kuhudhuria mikutano na kuwazungumzia wafadhili na washirika bila woga. Nimetokea kuwaheshimu sana wanawake wanashikilia nyadhifa za uongozi ninaokutana nao kwa sababu ninafahamu changamoto wanazokabiliana nazo wanawake katika uongozi. Nimeweza kuingiliana na wanawake wengine wanaoendeleza miradi mbalimbali na kujifunza mengi kutokana na ufanisi wao, na changamoto wanazokumbana nazo.

Kitu muhimu ambacho nimejifunza ni kuwa, kama mwanamke, ni vyema kutumia nafasi zetu za uongozi kuwafungulia njia wanawake wachanga ili nao waweze kujiendeleza. Napenda kuwatia moyo wanawake ninaofanya kazi nao kuhudhuria mikutano na kujieleza bila woga kwa sababu ninajua namna wanawake wachanga wanavyoweza kudhalilishwa, kunyamazishwa na kukashifiwa. Kama wanawake wachanga, hatuhitaji kushindana wenyewe kwa wenyewe, bali kufanya kazi kwa pamoja ili kufikia kilele cha maendeleo, sio kwa ajili yetu tu bali pia kwa manufaa ya vizazi vijavyo.

 

#YoungWomenSay is a collaboration between SayItForward.org and The Torchlight Collective in support of International Youth Day 2018 and culminating on International Day of the Girl. This campaign features blogs from incredible young women from around the world, and is designed to harness the power of storytelling and social media to drive attention to the lived experiences, dreams, and aspirations of young women around the world

We invite you to follow Say It Forward on Twitter, Facebook, and Instagram… and follow The Torchlight Collective on Facebook, Twitter and their hashtag #TheTorchlightCollective.

Story shared by...

Christine Sayo